Watoto wawili wafariki katika mkasa wa moto Laikipia

Dismas Otuke
2 Min Read

Simanzi imetanda katika kijiji cha Chung’uti kilichoko eneo la Muhotetu, Wadi ya Marmanet, Kaunti ya Laikipia, baada ya mkasa wa moto wa kutisha kuwaua watoto wawili wadogo asubuhi ya Jumatatu.

Kulingana na kumbukumbu za polisi zilizosajiliwa chini ya OB 03/04/08/2025 saa 6:30 mchana, moto huo ulizuka mnamo saa 4:00 asubuhi katika nyumba ya Bw. Waweru Mwangi. Naibu Chifu wa Muhotetu, Bw. Benjamin Wambugu, aliripoti kuwa alipokea simu ya dharura kutoka kwa mkazi aliyemuarifu kuhusu moto huo.

Maafisa wa polisi kutoka kituo cha eneo hilo, wakiongozwa na OCPD wa Laikipia Magharibi Bw. Francis Ng’ang’a, walifika haraka eneo la tukio. Walipowasili, walithibitisha vifo vya watoto wawili waliokuwa wamenaswa ndani ya nyumba hiyo. Wahasiriwa walitambuliwa kama Wanjiru mwenye umri wa miaka 3 na Charles Mubia mwenye umri wa miaka 7.

Chanzo cha moto bado hakijajulikana. Maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Kaunti Ndogo ya Laikipia Magharibi walifika na kuchunguza eneo la tukio kama sehemu ya uchunguzi unaoendelea. Miili ya marehemu ilisafirishwa hadi Hifadhi ya Maiti ya Nyahururu ambako uchunguzi wa maiti unatarajiwa kufanyika.

MCA wa Wadi ya Marmanet, Mhe. Simon Kanyutu, alizuru familia iliyoathirika na kutoa pole zake za dhati, akieleza tukio hilo kama “janga kubwa.” Aliwataka viongozi wa eneo na wahisani kuungana kuwasaidia waathiriwa.

“Hili ni pigo kubwa kwa jamii nzima,” alisema Mhe. Kanyutu. “Natoa wito kwa viongozi wenzangu kushirikiana nami kutoa msaada wa kihisia na mali kwa familia iliyopoteza wapendwa wao.”

Polisi wameanzisha uchunguzi rasmi kuhusu tukio hilo. Kesi hiyo inasimamiwa na ofisi ya DCI katika Laikipia Magharibi.

Share This Article