Biwi la simanzi lilitanda leo Jumatatu, baada ya watoto watatu kuteketea hadi kufariki ndani ya nyumba yao, katika kijiji cha Kahuho, Kaunti ya Kiambu.
Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi wa eneo la Kabete Anthony Mbogo, alisema watoto hao ni wa umri wa miaka 2,5 na 14.
Kulingana na Mbogo, moto huo ulisambaa kwa kasi na kuteketeza nyumba mbili za makazi, huku hali hiyo ikichangiwa na kuchelewa kufika kwa gari la zima moto la kaunti ya Kiambu.
Taarifa za awali zinaonyesha kuwa moto huo ulisababishwa na mlipuko wa mtungi wa gesi.
Boniface Mwangi, baba wa watoto hao walioangamia, alisema licha ya juhudi kubwa za majirani na watu wenye mapenzi mema kuzima moto huo, hazikufanikiwa.
Mwakilishi wadi wa eneo hilo Kamau Thumbi aliitaka serikali ya kaunti kutimiza ahadi yake ya kutoa gari la zima moto kwa eneo hilo, ambayo ilitolewa miaka miwili iliyopita.