Maafisa wa upelelezi wa jinai DCI wametangaza kukamatwa kwa watu watatu kwa tuhuma za kuendeleza kilomo cha bangi.
Watatu hao wanaojumuisha raia wawili wa kigeni walikamatwa katika kijiji cha Mwabungo huko Diani, katika kaunti ya Kwale kufuatia opEresheni iliyotekelezwa na maafisa wa vitengo mbalimbali.
Maafisa hao wakiongozwa na afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha Diani walitekeleza operesheni inayolenga upanzi haramu wa mihadarati.
Taarifa za ujasusi walizokuwa wamepokea ziliwaelekeza hadi eneo la Romika ambapo waligundua shamba la bangi.
Washukiwa hao ni mama kwa jina Wegener Geb Sikora wa umri wa miaka 66, mwanamume aitwaye Heck Klaus Edmund mwenye umri wa miaka 69 wote raia wa Ujerumani walio na viza za watalii na Anastasia Wangare mwenye umri wa miaka 27.
Walipatikana katika shamba hilo na wakatiwa mbaroni kabla ya kuwasilishwa kwa kitengo cha kukabiliana na mihadarati katika eneo la Pwani kwa uchunguzi zaidi.
Wakati huo huo uchunguzi katika shamba hilo la bangi umetekelezwa na ushahidi kukusanywa kwa ajili ya kuwashtaki mahakamani.