Watano wajeruhiwa baada ya afisa kufyatua risasi kimakosa mahakamani

Martin Mwanje
1 Min Read

Watu watano walijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini baada ya afisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI Konstebo Cornellious Murey kufyatua risasi kimakosa kutoka kwenye bastola yake wakati wa kusikilizwa kwa kesi mahakamani mjini Bungoma. 

Risasi hiyo ilimjeruhi Murey, afisa wa Idara ya Magereza na raia watatu.

“Wote watano walikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Bungoma wanakotibiwa. Wote wameripotiwa kuwa katika hali thabiti. Hakuna majeraha mabaya yaliyotokea wala kifo,” imesema Idara ya Mahakama kupitia msemaji wake Paul Ndemo kwenye taarifa.

“Maafisa wote wa mahakama na pia raia waliokuwa mahakamani wako salama na kwa hivyo hakuna haja ya kutaharuki.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, timu ya usalama ya kaunti imezuru eneo la tukio na inatathmini hali hiyo.

Kwenye taarifa, DCI ilithibitisha tukio hilo lililotokea majira ya saa saa 4:50 asubuhi leo Jumanne ikiongeza kuwa inashirikiana na Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi (IPOA) na Idara ya Mahakama katika uchunguzi wa kubaini hali iliyosababisha kutokea kwa tukio hilo.

Share This Article