Watalii wa kigeni milioni 2.4 ambayo ni rekodi waliitembelea Kenya mwaka 2024, na kuzidi idadi ya juu ya watalii walioripotiwa kuitembelea nchi hii miaka iliyopita.
Hii kwa mujibu ripoti ya utendakazi wa sekta hiyo ya mwaka 2024 iliyotolewa leo Jumatano na Waziri wa Utalii na Wanyamapori Rebecca Miano.
Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 15 ikilinganishwa na watalii milioni 2,089,259 walioitembelea Kenya mnamo mwaka 2023.
Aidha, kulikuwa na ongezeko la asilimia 19.79 la mapato yaliyotokana na ziara za watalii hao, yakipanda kutoka shilingi bilioni 377.49 mwaka 2023 hadi shilingi bilioni 452.20 mwaka 2024.

Sekta ya utalii wa ndani ya nchi pia ilionekana kuimarika huku idadi ya watalii wanaolala katika maeneo mbalimbali ya kitalii ikipanda kwa asilimia 12 kutoka milioni 4,618,094 mwaka 2023 hadi milioni 5,173,966 mwaka jana.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Mombasa, Waziri Miano alisema takwimu zinadhihirisha hatua za kimkakati zinazochukuliwa na serikali kuifufua sekta ya utalii nchini.
“Mafanikio haya ya taratibu ni matokeo ya hatua madhubuti za kimkakati zinazojumuisha kampeni za kuinadi nchi, utoaji ulioongezeka wa bidhaa anuai za kitalii, utumiaji wa majukwaa ya kidijitali na uanzishaji wa safari mpya zilizopangwa za ndege,” alisema Miano.
Watalii wengi walitokea nchini Marekani (12.8% ) ikifuatwa na nchi jirani za Tanzania (8.4%) na Uganda (9.4%).
Waziri Miano ameahidi kukuza ushirikiano zaidi wa sekta ya umma na kibinafsi na pia kutekeleza sera na mipango ambayo itachangia ukuaji endelevu wa sekta ya utalii nchini.