Wasichana nchini Uganda wameonywa wajihadhari na wanakandarasi wa kigeni wanaotekeleza miradi mbali mbali nchini humo.
Haya yanajiri kufuatia idadi kubwa ya wasichana wa taifa hilo wanaopachikwa mimba na wafanyakazi hao ambao wengi ni wa ujenzi wa miundombinu.
Msemaji wa wizara ya masuala ya ndani nchini Uganda Simon Mundeyi, amefichua kwamba katika muda wa wiki mbili pekee, wasichana 16 wamefika kwenye afisi za wizara hiyo kutafuta usaidizi.
Walitiwa mimba na raia hao wa kigeni ambao huwatelekeza punde wanaporejea kwenye nchi zao. Kulingana na Mundeyi wengi wa wasichana hao hawafahamu majina, uraia na hata habari nyingine kuhusu wanaume hao.
Msemaji huyo anaelezea kwamba wasichana hao walihadaiwa na ahadi za kupatiwa pesa na imani kwamba serikali ingewasaidia iwapo wangepata ujauzito.
Hata hivyo kina dada hao wameachwana watoto bila usaidizi wowote huku wakiwa hawana njia ya kupata haki.
Wizara hiyo ya masuala ya ndani ilifanya uchunguzi kuhusu kampuni za kigeni zinazounda barabara za Uganda na ikagundua kwamba wengi wa wafanyakazi hao walikuwa wafungwa wanaoendelea kuhudumia vifungo vyao kwenye nchi yao.
Matukio haya yameibua wasiwasi kuhusu hali ya wasichana wadogo wa Uganda ambao huenda wakapotoshwa na kujipata kwenye mahusiano na raia wa kigeni ilhali hawawaju.