Maafisa wa kituo cha polisi cha Busia wamewakamata washukiwa wawili wa ulanguzi wa bangi katika mji huo na viunga vyake.
Maafisa hao walinasa pikipiki yenye nambari ya usajili KMEY 867L na kumkamata mwanamume mwenye umri wa miaka 50 kwa jina Alfred Ouma Mapesa aliyekuwa akiiendesha.
Walipokagua gunia alilokuwa amebeba, walibaini gunia hilo lilikuwa na kilo 24 za bangi.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inasema Mapesa alipohojiwa, alifichua mshirika wake kwenye biashara hiyo ambaye ni Frederick Egesa Wafula mwenye umri wa miaka 41.
Wafula alikamatwa baadaye na kupelekwa kizuizini.
Wawili hao wanazuiliwa na maafisa wa polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.