Washukiwa wawili wa ugaidi wahukumiwa miaka 30 gerezani

Tom Mathinji
2 Min Read
Washukiwa wa Ugaidi wahukumiwa miaka 30 gerezani.

Washukiwa wawili wa ugaidi wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kufanikisha shambulizi la kigaidi kwenye hoteli ya Dusit D2 Jijini Nairobi mwaka 2019.

Mahakama ya kushughulikia kesi za ugaidi ya Kahawa, imemhukumu Mohamed Abdi Ali mwenye umri wa miaka 61, miaka 15 gerezani kwa kuunga mkono shughuli za kigaidi na miaka zingine 15 gerezani kwa kupanga kutekeleza uhalifu kinyume na sehemu za 23(2) na 23(4) ya sheria za kuzuia ugaidi.

Wakati huo huo, mahakama hiyo ilimfunga jela Hussein Mohamed Abdille miaka 15 gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kupanga shambulizi la kigaidi, na miaka zingine 15 kwa kufanikisha ugaidi.

Wawili hao walihusishwa na shambulizi la kigaidi lililotekelezwa katika hoteli ya Dusit D2 Januari 15,2019, ambapo watu 21 walipoteza maisha, huku wengine wakipata majeraha.

Akitoa hukumu hiyo Alhamisi, Lady Justice Diana Kavedza alisema mahakama iliridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, na kudhibitisha kesi dhidi ya Hussein Mohamed Abdille na Mohamed Abdi Ali bila tashwishi.

Lady Justice Kavedza, katika hukumu yake alidokeza kuwa Wakenya bado wanakumbuka woga, uchungu na usumbufu wa kimawazo lakini pia ujasiri wa waliopoteza maisha yao, walipoteza kazi, biashara na wale walio na majeraha, na kwamba hukumu yake inazungumza kwa niaba ya walionusurika katika shambulizi hilo.

Baada ya kuwasilisha ushahidi mahakamani, upande wa mashtaka uliitaka mahakama kuwahukumu kufungo cha juu zaidi washtakiwa hao, na kwamba vifungo vyao viandamane pamoja.

Share This Article