Maafisa wa polisi wamewatia nguvuni washukiwa wanne wakiwemo raia wawili wa kigeni, kwa kutoa vyeti ghushi vya shahada ya uzamili katika hoteli moja Jijini Mombasa.
Washukiwa hao Dayis Lawrence Bennett raia wa Marekani, Farah Akab raia wa Pakistan na wakenya Ekra Ndung’u na Josephine Ndune, walikamatwa wakikabidhi wanafunzi vyeti hivyo baada ya kuwapa mafunzo ya siku tatu pekee.
Walikamatwa baada ya maafisa wa polisi kuwafumania katika hoteli hiyo, sherehe ya kuwatawaza wanafunzi vyeti hivyo ilipokuwa ikiendelea.
Baadaye washukiwa hao walifikishwa katika mahakama ya Shanzu, ambako walikanusha mashtaka ya kutoa vyeti vya masomo kinyume na sheria za vyuo vikuu.
Waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 400,000, huku vyeti vyao kwa usafiri vya raia hao wawili wa kigeni vikizuiliwa na mahakama. Kesi dhidi yao itatajwa Februari 18, 2025.