Washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati, pombe haramu wakamatwa Kakamega

Martin Mwanje
1 Min Read

Washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati na utengenezaji wa pombe haramu wamekamatwa katika maeneo ya Sigalagala, Maseno, na Shinyalu katika kaunti ndogo ya Kakamega Kusini. 

Wote hao walikamatwa wakati wa operesheni ya pamoja iliyofanywa na maafisa kutoka Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS kwa kushirikiana na maafisa kutoka Mamlaka ya Taifa ya Kupambana na Mihadarati na Pombe Haramu, NACADA.

Wakati wa operesheni hiyo, maafisa hao walimkamata mshukiwa mkuu anayetuhumiwa kwa kuwauzia bangi wanafunzi katika eneo hilo.

Mshukiwa huyo alipelekwa katika kituo cha polisi cha Kakamega akisubiri kuandikisha taarifa na kufikishwa mahakamani.

Maafisa pia walivamia maeneo matano makuu ya utengenezaji wa pombe haramu kando ya mto Yala na kuharibu zaidi ya lita 5,000 za pombe aina ya chang’aa na zaidi ya lita  100,000 za pombe inayotengenezwa katika eneo hilo kwa jina “Sigalagala.”

Mshukiwa mmoja anayehusishwa na utengenezaji huo pia alikamatwa na anasubiri kufunguliwa mashtaka.

 

Share This Article