Washukiwa watatu wa ugaidi ambao ni Wakili Andrew Chacha Mwita, Mariam Ali Abdalla na Stephen Kiveve Musembi, jana walifikishwa katika mahakama ya Kahawa.
Watatu hao walikuwa mbele ya jaji Gideon Kiage wakikabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ugaidi kama kukusanya mali na kutoa mali na huduma kwa ajili ya vitendo vya kigaidi.
Kosa jingine ni kuhusika na mali inayomilikiwa au kusimamiwa na makundi ya kigaidi.
Wakili Mwita anatuhumiwa kusaidia kuhamisha fedha kutoka akaunti ya ‘cryptocurrency’ inayohusishwa na kundi la kigaidi la Islamic State East Africa kupitia akaunti yake ya M-Pesa.
Mshukiwa huyo alipokea dhamana ya kibinafsi ya shilingi milioni 5 na kuhitajika kutoa watu wawili kwa ajili ya mawasiliano.
Kesi yake itatajwa Januari 20, 2026.
Mariam Ali Abdalla vile vile anatuhumiwa kwa kuhusika na mali inayomilikiwa na makundi ya kigaidi. Anaripotiwa kusaidia kuhamisha fedha za kundi la Islamic State mnamo Agosti 22, 2024, kupitia akaunti yake ya Mpesa.
Alikanusha mashtaka dhidi yake huku upande wa mashtaka ukipinga ombi lake la dhamana. Alirejeshwa rumande katika gereza la wanawake la Lang’ata akisubiri uamuzi wa ombi la dhamana Disemba 8, 2025.
Stephen Kiveve Musembi naye anatuhumiwa kwa makosa sawia na alikanusha mashtaka dhidi yake mahakamani. Kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Kamiti.
Disemba 15, 2025, mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu ombi la Musembi la dhamana huku maandalizi ya ripoti yake kuhusu kipindi cha majaribio kabla ya dhamana.