Maafisa wa usalama wamewakamata washukiwa sita wa ubakaji katika kaunti ya Meru.
Washukiwa hao wanadaiwa kutekeleza uovu huo Disemba 1, 2025 katika eneo la Laare, kaunti ndogo ya Igembe Kaskazini, kaunti ya Meru.
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wakazi waliripoti kisa cha mwanamke ambaye alikuwa akibakwa kwa zamu na kundi la wanaume waliokuwa wakishiriki katika shughuli ya upashaji tohara kwa njia ya kitamaduni.
Maafisa wa polisi walichukua hatua za haraka na kumuokoa mwanamke huyo, kabla ya kumpeleka kwenye kituo cha afya cha Nyambene kwa matibabu, huku wakianzisha msako dhidi ya washukiwa hao.
DCI ilisema kuwa maafisa hao walitekeleza msako katika maeneo ya Irinde, Lubwa na Kiarama, na kufanikiwa kuwatia nguvuni Dennis Mwirigi, Ismael Gichuge, Elijah Muriki, Isaac Ntomauta, Joseph Marete na Phineas Mutali.
Washukiwa hao wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi, wakisubiri kufikishwa mahakamani.