Washukiwa sita wanaodaiwa kuhusika katika kisa ambapo afisa wa polisi alipigwa risasi na kufariki mnamo Juni 18,2025 kwenye makutano ya Thika na Garissa, wamekamatwa.
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), maafisa wa polisi walitumia mbinu za kisayansi kuwatambua washukiwa hao na kuanzisha operesheni iliyofanikisha kukamatwa kwao katika mtaa wa Kahawa West.
Washukiwa hao ni pamoja na Joseph Ngotho Karanja, Benjamin Kambo Mwangi, Athanase Ndacaisaba, Kelvin Mbilika Ollingo na Samuel Omurambi. Mshukiwa wa sita Philip Muiruri Muchiri, alikamatwa katika mtaa wa Kiamumbi.
Maafisa hao walipata gari linaloshukiwa kutumiwa na washukiwa hao katika visa vya uhalifu, lenye nambari za usajili KDQ 529W.
Sita hao walifikishwa katika mahakama ya Thika, ambapo maafisa wa polisi walipata kibali cha kuwazuilia kwa siku 21 ili kuwapa fursa kuendelea na uchunguzi.
Kesi hiyo itatajwa Agosti 11, 2025.