Washukiwa 14 wamekamatwa kuhusiana na uharibifu na wizi wa mali uliotekelezwa wakati wa msako ulioendeshwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), katika makao ya Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) siku ya Alhamisi, ilisema hatua ya kuwazuia maafisa wa EACC kufanya uchunguzi ilikiuka sheria.
“Kundi la maafisa kutoka asasi mbali mbali likiongozwa na maafisa wa usalama kutoka eneo hilo kwa usaidizi wa wale kutoka makao makuu ya DCI, lilitekeleza operesheni na kuwakamata washukiwa 14 wanaohusishwa na uharibifu na wizi wa mali katika makazi ya Gavana wa Trans Nzoia,” ilisema taarifa ya DCI kupitia ukurasa wa X.
DCI ilidokeza kuwa msako dhidi ya washukiwa zaidi unaendelea, wakiwemo waliofadhili na kupanga tukio hilo la siku ya Jumanne wiki jana.
Tume ya EACC imekashifu uvamizi huo dhidi ya maafisa wake pamoja na kuharibiwa kwa magari yao.
Washukiwa waliotiwa nguvuni ni pamoja na Leon Ikua, Brian Mutonyi, James Maina, Churchill Ambula, Chirispus Kingara, Joseph Kakanja, Daniel Kanyingi, Levy Kiprotich, John Kamau, Benjamin Bukhala, Lavingtone Kipkemboi, Isaac Nyongesa Wanyonyi Wasike, Tonny Wafula Wasike na Ismael Juma.