Washukiwa 11 wakamatwa kwa kushiriki biashara haramu ya dhahabu

Tom Mathinji
1 Min Read
Maafisa wa DCI wanasa kilo 350 za dhahabu bandia.

Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wamewakamata washukiwa 11 na kupata kilo 350 za dhahabu bandia katika mtaa wa Spring Valley, Jijini Nairobi.

Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa hao waliwafumania washukiwa hao na kuwapata na kilo 350 za dhahabu bandia, mashini ya kupima uzani na kifaa cha kieletroniki cha kuchunguza dhahabu almaarufu Tester Gun.

Maafisa hao pia walipata stakabadhi kadhaa pamoja na koti iliyokuwa na nembo ya Wizara ya Madini, inayodaiwa ilitumika kuwahadaa watu wakati wa kutekeleza ulaghai.

Washukiwa hao wanajumuisha raia saba wa Kenya ambao ni Allan Zephaniah Onyango, Nicodemus Okoth, Phillip Onyango, Elmad Ochola, Shem Omollo, Edward Leonard Ochieng, na James Jeremiah Akumu, raia wawili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nfundiko Kamira na Lukabaya Mulamba, na raia wawili wa Cameroon Ibrahim Nzamgou naMike Fouapon.

Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill, wakisubiri kufikishwa mahakamani.

TAGGED:
Share This Article