Wasanii na washawishi waliokwenda Israel wakashifiwa

Marion Bosire
2 Min Read

Wasanii, watu maarufu na washawishi wa mitandaoni wa Kenya waliokubali safari ya bure kuelekea Israel sasa wanakashifiwa vikali na wanamitandao.

Waliosafiri kuelekea nchi hiyo ni pamoja na waimbaji wa nyimbo za injili Kambua na Evelyn Wanjiru ambao wamekuwa wakichapisha picha na video za matukio ya ziara hiyo.

Wengine ni pamoja na Kestin Mbogo, Caleb Karuga, Mwende Macharia, Gadwilliam Kiragu, Mimo Karanja na Sim Simmer.

Waandalizi wa ziara hiyo ambao wanaaminika kuwa serikali ya Israel walilipia wakenya hao safari za ndege za kwenda na kurudi, malazi na chakula huku wakiwataka wanakili picha na video za waliyoyaona huko na kuchapisha mitandaoni.

Machapisho yao ndiyo yaliwafanya watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini kufahamu kilichokuwa kikiendelea.

Wasanii hao pamoja na washawishi wanakosolewa vikali ikitizamiwa kwamba ziara hiyo imejiri wakati ambao mzozo kati ya Israel na Gaza unaendelea huku wao wakionekana wenye furaha katika safari hiyo.

Kambua jana aliandika kuhusu aliyokutana nayo jijini Jerusalem akiyataja kuwa ya kubadili maisha. Alizuru maeneo kama Golgotha, kaburi la yesu na mji wa kale ambayo kulingana naye yanahuisha yale ambayo amekuwa akisoma kwenye Biblia.

Evelyn Wanjiru alisimulia kuhusu eneo la jangwa la Kibbutz Kalia ambalo limegeuzwa na kuwa eneo la uzalishaji wa chakula akisifia ubunifu na ustahimilivu alioshuhudia.

Gadwilliam Kiragu ambaye muunda maudhui mitandaoni alitaja muda wake katika jiji ‘takatifu’ la Jerusalem kuwa jambo lisilosahaulika milele.

Mtangazaji wa redio Mwende Macharia alikutana na Chen Malka, aliyenusurika shambulizi la kigaidi kwenye tamasha la Nova mwaka 2023 ambapo watu 400 waliuawa.

Mkewe mwanamuziki Kaymo ambaye anaitwa Rachel alichapisha video kwenye mitandao ya kijamii akielezea kwamba yeye na muwe wake pia walialikwa kwenda ziara ya Israel lakini wakaamua kususia.

Rachel anaelezea kwamba waandalizi walitaka kutangaza uzuri wa Israel na kulingana naye, hakuna lolote zuri kuhusu nchi hiyo.  Anahisi waliokubali walihadaika na majukwaa yao yanatumika vibaya.

Share This Article