Bingwa wa Olimpiki Emmanuel Wanyonyi, alisajili ushindi wa mbio za mita 800 katika mkondo wa Uswidi wa Diamond League jana usiku, akiweka muda wa kasi ulimwenguni mwaka huu wa dakika 1 sekunde 41.95.
Wanyonyi anayelenga kuhifadhi taji yake ya Diamond, alikimbia muda huo wa kasi kwa mara ya kwanza tangu mashindano ya dunia ya mwaka 2023 mjini Budapest.
Djame Sedjati wa Algeria alimaliza wa pili kwa dakika 1 sekunde 42.27, huku Josh Hoey wa Marekani akiambulia nafasi ya tatu kwa dakika 1 sekunde 42.43.
Bingwa wa Dunia Mary Moraa alimaliza wa pili katika mita 800 akiweka muda bora wa kibinafsi wa dakika 1 sekunde 57.83 nyuma ya George Hunter, wa Uingereza aliyeibuka mshindi kwa dakika 1 sekunde 57.66.
Prudence Sekgodiso wa Afrika Kusini alimaliza wa tatu.
Mkondo ujao wa nane wa Diamond League utaandaliwa Julai 20 jijini Paris, Ufaransa.