Wanne wauawa katika shambulizi kanisani Michigan

Marion Bosire
3 Min Read

Angalau watu wanne wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mshambuliaji kuendesha gari na kuingia ndani ya kanisa moja huko Michigan, kufyatua risasi na kuliteketeza kwa moto, haya ni kulingana na maafisa wa polisi.

Maafisa walisema shambulio hilo lilitokea katika Kanisa la Yesu Kristo wa Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Grand Blanc, mji ulio umbali wa kilomita 100 kaskazini-magharibi mwa Detroit, wakati wa ibada ya Jumapili iliyohudhuriwa na mamia ya watu.

Mtuhumiwa, aliyetambuliwa kama Thomas Jacob Sanford, wa umri wa miaka 40 kutoka Burton, Michigan, alipigwa risasi na kuuawa na polisi katika maegesho ya kanisa hilo.

Mamlaka zinalichukulia tukio hilo kama kitendo cha vurugu kilichopangwa lakini wanasema bado sababu ya shambulio haijafahamika.

Kamanda wa Polisi wa mji wa Grand Blanc William Renye, aliambia waandishi wa habari Jumapili kwamba waathiriwa wawili walikufa kwa majeraha ya risasi.

Moto huo ulisababisha uharibifu mkubwa kwa jengo hilo na baadhi ya watu bado hawajulikani walipo kulingana na Kamanda Renye.

Awali, alisema kuwa mamia ya watu walikuwa wakihudhuria ibada saa nne na dakika 25 asubuhi kwa saa za huko wakati mshambuliaji aliendesha gari kuingia kanisani.

Mshambuliaji huyo kisha alianza kufyatua risasi kwa bunduki ya kijeshi ambapo alifyatua risasi kadhaa kwa watu waliokuwa ndani ya kanisa.

Polisi walifika haraka kwenye eneo la tukio na kurushiana risasi na mtu huyo kabla ya kumdhibiti. Alipigwa risasi na kuuawa saa 4:33 asubuhi, dakika nane baada ya risasi kuanza.

“Tunajaribu bado kubaini hasa moto ulitokea wapi na ulianzaje,” alisema kamanda huyo. “Hata hivyo, tunaamini ulianzishwa makusudi na mshukiwa.”

Kamanda Renye pia aliwasifu waumini kwa ujasiri wao kwa kuhifadhi watoto kanisani wakati wa tukio hilo.

Wachunguzi wanakagua mali ya mshukiwa na rekodi za simu yake ili kujaribu kuelewa sababu ya tukio hilo.

FBI inaongoza uchunguzi huo na imetuma vikosi vya kukabiliana na dharura, wataalamu wa mabomu na maafisa wengine kwenye eneo la tukio, kwa mujibu wa Reuben Coleman, kaimu wakala maalum wa ofisi ya FBI ya Detroit.

Rais Donald Trump alisema amefahamishwa kuhusu shambulio hilo, na alithibitisha kuwa FBI itaongoza uchunguzi wa serikali kuu.
Kupitia mtandao wa Truth Social, alitaja tukio hilo kama shambulio lingine lililolenga Wakristo nchini Marekani.

Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Pam Bondi, alisema kwenye mtandao wa X kuwa amepokea taarifa kuhusu shambulio la kutisha la risasi na moto katika kanisa hilo.

“Vurugu kama hii katika sehemu ya ibada ni ya kuhuzunisha na ya kutisha,” alisema Bondi. “Tafadhali ungana nami kuwaombea waathiriwa wa janga hili la kusikitisha.”

Gavana wa Michigan, Gretchen Whitmer, alilaani tukio hilo, akisema Vurugu kokote hasa katika sehemu ya ibada haikubaliki na akaongeza kuwa anafuatilia hali hiyo.

Share This Article