Watu wanne walithibitishwa kufariki na wengine zaidi ya 20 kukimbizwa hospitalini, kufuatia ajali ya moto kaika hoteli ya Sunrise, kwenye barabara ya Khamis, jijini Kampala nchini Uganda.
Kufikia jana adhuhuri magari ya kusafirisha wagonjwa yanayomilikiwa na polisi na jeshi la Uganda yalionekana yakipeleka waathiriwa hospitalini.
Kulingana na mmoja wa walioshuhudia ajali hiyo, mmoja wa waliofariki alikuwa mgeni kwenye hoteli hiyo ambaye alitanguliza kichwa alipokuwa akiruka kutoka kwenye chumba cha hoteli hiyo kukwepa moto.
Waziri wa mamlaka ya jiji kuu Kampala Minsa Kabanda alithibitisha ajali hiyo huku akihimiza wamiliki wa majengo kuhakikisha wanaweka vifaa vya kuzima moto.
Magari yaliyokuwa yameegeshwa nje ya hoteli hiyo yaliharibika kabisa na vijana wa mitaani walionekana wakijizolea mabaki ya magari hayo.
Meya wa jiji la Kampala Erias Lukwago naye alilalamikia uwezo wa huduma ya taifa hilo ya kuzima moto suala alilosema linastahili kushughulikiwa haraka.
Alisema moto huo ulizuka mapema asubuhi jana na kufikia saa sita haukuwa umethibitiwa ishara kwamba kuna mapungufu katika idara ya zima moto.
Mkuu wa polisi katika eneo la Kampala mjini Moses Nanoka alifika katika eneo la tukio ili kusaidia kudhibiti hali.