Wanawake wa ACK Isiolo waandamana kulalamikia ongezeko la uhalifu

Martin Mwanje
3 Min Read

Wanawake kutoka Kanisa la Kianglikana (ACK) katika kaunti ya Isiolo wameandaa maandamano ya amani kulalamikia ongezeko la visa vya uhalifu mjini Isiolo na maeneo ya karibu, hali ambayo imewatia hofu wakazi. Hii ni hasa baada ya kifo cha mmoja wao, Nelly Elibate, aliyeuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake katika kijiji cha Kambi ya Juu wiki moja iliyopita.

Katika shambulizi hilo la usiku, wahalifu hawakuiba chochote ila walijeruhi pia ng’ombe wake wawili kwa risasi.

Siku tatu zilizopita, Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Kisomali, Idle Hassan, alipigwa risasi mara kadhaa nje ya Msikiti wa Jamia mjini Isiolo alipokuwa akielekea kwa sala ya jioni. Kwa bahati nzuri, alinusurika na kwa sasa anapokea matibabu katika hospitali moja mjini Meru.

Wanawake hao, waliokuwa chini ya mwavuli wa Muungano wa Kina Mama wa Kanisa la Anglikana (ACK) Dayosisi ya Marsabit, wakiongozwa na Mratibu wao Mchungaji Elema, walilalamikia mwitikio hafifu na wa polepole wa vyombo vya usalama wa serikali katika kudhibiti ongezeko la uhalifu, jambo linalotishia kuvuruga amani na mshikamano wa kijamii uliodumu kwa muda mrefu miongoni mwa wakazi wa Isiolo.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika laIsiolo Gender Watch, Grace Lolim, alielezea wasiwasi wake kuhusu mwelekeo mpya wa uhalifu, akisema kuwa tofauti na hapo awali ambapo visa vya wizi wa mifugo vilihusisha mapigano vijijini, sasa watu wanapigwa risasi hata katikati ya mji wa Isiolo na maeneo ya makazi kama Kambi ya Juu, ambako Nelly aliuawa.

Wanawake hao walifanya maandamano ya amani kutoka Kanisa la Uhuru ACK katika wadi ya Burat, wakipitia katikati ya mji wa Isiolo hadi Kanisa la ACK eneo la Mwangaza, ambako walifanya mkutano na wanahabari. Walitoa wito kwa vyombo vya usalama vya serikali kuongeza juhudi za kulinda maisha na mali ya wananchi, na kuhakikisha wahalifu wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria ili kumaliza wimbi hilo la uhalifu.

Lolim pia alitoa wito kwa serikali kuongeza ajira na usambazaji wa polisi wa akiba ili kusaidia kuimarisha usalama katika vijiji.

Marehemu Nelly, ambaye pia alikuwa mke wa mchungaji wa Kanisa la ACK, ameacha nyuma watoto wanne wadogo.

Dayosisi ya ACK ya Marsabit inasimamia pia kaunti ya Isiolo na maeneo ya kaunti ya Samburu.

Share This Article