Wanasiasa wanaowapa vijana mihadarati mashakani

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa usalama wa taifa Kipchumba Murkomen.

Serikali imetoa onyo kali kwa wanasiasa wanaowapatia vijana pombe na mihadarati, ikisema hatua hiyo inahujumu kampeni za kupambana na uraibu wa mihadarati hapa nchini.

Akizungumza leo Alhamisi wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwaka 2024 kuhusu utumizi wa mihadarati katika taasisi za elimu ya juu, waziri wa usalama wa taifa Kipchumba Murkomen alisema serikali itawachukulia hatua kali za kisheria wanasiasa watakaopatikana wakiwapatia vijana pombe na mihadarati.

Waziri huyo alisema serikali imeimarisha kitengo cha kukabiliana na mihadarati, ili kutokomeza uraibu huo ambao unasambaratisha maisha ya siku za usoni za vijana hapa nchini.

“Vile vile tunaweka mikakati mingine ya kuimarisha uwezo wa vituo vya polisi karibu na taasisi za elimu ya juu kuwezesha ukusanyaji habari za kijasusi na ushirikiano na asasi zingine kukabiliana na uraibu huo,” alisema Murkomen.

Alidokeza kuwa vyuo vikuu vinapaswa kuwa salama kwa vijana, huku akiwataka wazazi kufuatilia mienendo ya wanao kila mara.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Halmashauri ya kitaifa ya kukabiliana na uraibu wa Pombe na Mihadarati  NACADA, ilidokeza kuwa uvutaji bangi ni uraibu  unaotumiwa zaidi na wanafunzi wa vyuo vikuu kwa asilimia 61.7, ukifuatwa na vyakula vinavyoliwa na vinywaji vilivyowekwa bangi kama vile sharubati kwa asilimia 47.6.

Share This Article