Wanasiasa waonywa dhidi ya matamshi yanayohujumu uuzaji Majani Chai Sudan

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri Kinyanjui awaonya wanasiasa dhidi ya matamshi yanayoweza hujumu uuzaji Majani Chai Sudan.

Waziri wa biashara Lee Kinyanjui, amewaonya wanasiasa dhidi ya kutoa matamshi yanayoweza hujumu uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Sudan.

Kinyanjui alisema matamshi ya kiholela yanaweza sambaratisha uuzaji wa Majani Chai nje ya nchi na hivyo kuwaathiri wakulima wa zao hilo.

Akizungumza baada ya mashauriano na mwenzake wa Ethiopia Dkt. Kassahun Gofe Jijini Mombasa, Kinyanjui alisema Sudan inasalia kuwa soko muhimu kwa Majani Chai ya Kenya, na matamshi ya kiholela ya wanasiasa kuhusu Mambo ya Nje, yanaweza kuwa na athari kubwa ya kiuchumi kuhusu biashara.

“Sudan ni soko muhimu sana kwa Majani Chai kutoka Kenya. Iwapo viongozi wetu wataendelea kuingilia maswala ya kimataifa, wale watakaoathirika pakubwa ni wakulima kule vijijini,” alisema Kinyanjui.

Waziri huyo alielezea wasiwasi kuhusu matamshi ya hivi punde kutoka kwa baadhi ya wanasiasa kuhusu mzozo unaoghubika kanda hii, akisisitiza umuhimu wa kudumisha msimamo wa Kenya usioegemea upande wowote katika maswala ya kimataifa.

“Kenya huwaheshimu majirani wote, ikiwemo Sudan. iwapo kutazuka mzozo wa ndani na tuhitajike kusuluhisha, hatuegemei upande wowote,” alidokeza Kinyanjui.

Aidha waziri huyo alielezea juhudi za serikali za kuimarisha miundo mbinu ili kupiga jeki biashara, hasaa na Ethiopia.

Alisema bandari ya Lamu ina uwezo wa kuhifadhi meli kubwa na imo katika eneo nzuri la kuhudumia masoko ya Ethiopia kwa ufanisi mkubwa ikilinganishwa na njia zingine zilizopo.

Share This Article