Wanasheria kadhaa leo Ijumaa wameandamama jijini Nairobi kulalamikia mauaji ya mwanasheria mwenzao Kyalo Mbobu.
Wakiongozwa na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK, Faith Odhiambo, wanasheria hao waliovalia utepe wa zambarau wamezitaka asasi za upelelezi kuharakisha uchunguzi wa mauaji hayo na kuwawajibisha wahusika.
Maandamano yao yalianzia katika mahakama ya Milimani hadi jengo la Town House katikati ya jiji ziliko afisi za marehemu wakili huyo.
“Tunaziomba asasi za uchunguzi kuharakisha uchunguzi wao ili wahusika wa mauaji haya ya kikatili wawajibishwe,” alisema Odhiambo aliyeandamana na mwenyekiti wa Kamati ya Wanasheria Wabobezi, Philip Murgor miongoni mwa wanasheria wengine wengi.
“Tunatoa wito kwa vyombo vya habari pia kuziacha asasi za uchunguzi kukamilisha uchunguzi wao. Kukimbilia kukata kauli cha kilichotokea na kumchafulia sifa mwenda zake hakuwezi kuhalalisha mauaji haya ya kinyama,” alisihi Odhiambo.

Mwanasheria Mbobu alipigwa risasi na kuuawa papo hapo na watu wasiojulikana Jumanne jioni wiki hii.
Alikumbana na mauti akiwa kwenye gari lake mtaani Karen baada ya kuuawa na mtu aliyesemekana kuwa kwenye pikipiki.
Upasuaji wa maiti ulibaini jana Alhamisi kuwa marehemeu alifyatuliwa risasi 8 na kufariki kutokana na kuvuja damu nyingi.

Maafisa wa ujasusi wameanzisha uchunguzi kubaini kiini cha mauaji hayo ya kinyama kwa lengo la kuwawajibisha wahusika.
Mwanasheria huyo alikumbana na mauti wakati ambapo visa vya watu kupigwa risasi na kuuawa na watu wasiojulikana vimeongezeka nchini katika siku za hivi karibuni.
Mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were pia aliuawa na mtu aliyesemekana kuwa kwenye pikipiki jijini Nairobi.
Ikumbukwe kuwa aliyekuwa mbunge wa Kabete George Muchai pia aliuawa jijin Nairobi katika hali yiyo hiyo.