Naibu Inspekta Jenerali wa polisi Eliud Lagat, ametoa makataa ya saa 24 kwa wale wanaomiliki silaha kinyume cha sheria katika eneo la bonde la Kerio, kuzisalimisha mara moja.
Wakati huo huo, Lagat aliagiza kuimarishwa kwa operesheni za kuwatokomeza wahalifu wanaohujumu amani katika eneo hilo.
Lagat pia alifutilia mbali mikutano ya kiusalama inayotekelezwa na wazee wa vijiji, ili kutoa fursa kwa maafisa wa usalama kuendesha operesheni za kiusalama kikamilifu.
Alisema hayo alipozuru eneo la Tot linalokabiliwa na visa vya wizi wa mifugo, ambako aliandaa mikutano ya kiusalama na wawakilishi kutoka kaunti ndogo za bonde la Kerio, Pokot ya Kati na Tiaty.
Afisa huyo mkuu wa polisi alidokeza kuwa ongezeko la visa vya ukosefu wa usalama, limeshuhudiwa katika eneo hilo, ambapo watu watatu walipoteza maisha yao.
Lagat alihimiza jamii kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama kuwakamata wahalifu.
Watu wanne, wakiwemo wanafunzi wawili waliuawa hivi majuzi katika visa viwili tofauti vya ujangili katika kaunti za Elgeyo Marakwet na Baringo.