Polisi wamesema kwamba wanamaji wawili wa Marekani walioko Okinawa nchini Japan, wanachunguzwa kwa madai ya ubakaji, tukio la hivi karibuni katika msururu wa visa vya mashambulizi ambavyo vimeghadhabisha wakazi.
Marekani ina takriban wanajeshi 54,000 walioko Japan wengi wao wakiwa kwenye kisiwa cha kusini cha Okinawa, mashariki mwa Taiwan.
“Mwanamaji mmoja wa Marekani wa umri wa miaka 20 anashukiwa kubaka mwanamke raia wa Japan kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani mwezi Machi na anashukiwa pia kujeruhi mwanamke mwingine” afisa wa polisi wa eneo hilo aliambia shirika la habari la AFP.
Mwanamaji wa pili wa umri wa miaka 20 pia anashukiwa kumbaka mwanamke raia wa Japan katika kambi ya Marekani mwezi Januari, kulingana na afisa huyo.
Polisi wamekabidhi kesi hizo kwa waendesha mashtaka.
Balozi wa Marekani nchini Japan George Glass amesema kwamba nchi yake itashirikiana kikamilifu na mamlaka za Japan katika uchunguzi.
“Tunathamini sana mahusiano ya kuaminiana na urafiki tuliyojenga kwa miongo mingi na wenyeji wetu wa Japan na ninajitolea kufanya kila niwezalo kuzuia matendo ambayo yanaweza kuhatarisha uhusiano huu,” alisema Glass katika taarifa.
Ijumaa, wanajeshi wa Marekani walijiunga na maafisa wa Japan na wakazi wa Okinawa kwa doria ya usiku ya pamoja katika barabara ya mjini iliyojaa baa.
Doria hiyo ya kwanza ya aina hiyo tangu mwaka 1973 ilifuatia visa vingine vya ubakaji vilivyohusisha wanajeshi wa Marekani huko Okinawa.
Mwanamaji wa umri wa miaka 21 alishtakiwa kwa ubakaji mwezi Juni mwaka jana, miezi michache tu baada ya mwanajeshi wa Marekani wa umri wa miaka 25 kushtakiwa kwa madai ya kubaka msichana aliyekuwa na umri wa chini ya miaka 16.
Gavana wa Okinawa, Denny Tamaki, alitaja kesi hizo za hivi karibuni kuwa za kusikitisha sana akisema mamlaka zitalitaka jeshi la Marekani kuchukua hatua za kuzuia matukio kama hayo.
Msemaji mkuu wa serikali ya Japani, Yoshimasa Hayashi, alikataa kutoa maoni kuhusu kesi hizo katika mkutano wa kawaida na waandishi wa habari Alhamisi, lakini alisema uhalifu unaotekelezwa na wanajeshi wa Marekani haueleweki na haukubaliki.
Ubakaji wa mwezi Machi ulifanyika kwenye choo na mwanamke aliyejeruhiwa alikuwa akijaribu kuzuia shambulizi dhidi ya mwanamke mwingine kulingana na vyanzo vya polisi.
Uhusiano kati ya wakaazi wa Okinawa na kambi za Marekani umekuwa wa mkwaruzano kwa muda mrefu.
Mwaka jana, jumla ya watu 80 waliohusishwa na jeshi la Marekani walishtakiwa Okinawa kwa makosa mbalimbali kulingana na polisi.
Ubakaji wa pamoja wa msichana wa umri wa miaka 12 na wanajeshi watatu wa Marekani mwaka 1995 huko Okinawa uliibua hasira kubwa na kuibua wito wa kutathmini upya mkataba wa mwaka 1960 unaoruhusu Marekani kuweka wanajeshi wake nchini Japani.