Maafisa wakuu wa jeshi la Guinea-Bissau wakiongozwa na Brigedia Jenerali Denis N’Canha, wanasema wametwaa madaraka nchini humo huku rais akikamatwa.
Wanajeshi hao waliamuru kusitishwa kwa mchakato wa uchaguzi na kufungwa kwa mipaka siku moja kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.
Brigedia N’Canha na wenzake walitangaza hatua hiyo jana Jumatano Novemba 26, 2025 kupitia runinga, ambapo walijirejelea kama “Kundi kuu la Kijeshi la Kurejesha Utulivu”.
Walisema hali itasalia kuwa chini ya amri yao nchini humo hadi taarifa nyingine itakapotolewa.
Mipaka yote ya nchi hiyo kwa njia ya nchi kavu, angani na baharini imefungwa kwa muda usiojulikana na amri ya kutotoka nje usiku pia imewekwa.
Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya milio mikubwa ya risasi kusikika karibu na makao makuu ya tume ya uchaguzi, ikulu ya rais na Wizara ya Mambo ya Ndani katika mji mkuu, Bissau.
Matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili ambapo Rais Umaro Sissoco Embaló alikuwa anashindana na Fernando Dias yalitarajiwa kutangazwa leo Alhamisi katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Rais Embalo alihojiwa na kituo cha televisheni ya Ufaransa cha France24 kwa njia ya simu, ambapo alikiri kwamba ameondolewa madarakani na anazuiliwa katika makao makuu ya jeshi.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani PAIGC, Domingos Simões Pereira, pia amekamatwa na kuna fununu kwamba jeshi linajaribu kukata intaneti.