Wanajeshi waonywa dhidi ya ufisadi wakati wa usajili wa makurutu

Tom Mathinji
2 Min Read
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi (KDF), Jenerali Charles Kahariri.

Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi (KDF) Jenerali Charles Kahariri, amewaonya wanajeshi dhidi ya kujihusisha na ufisadi wakati wa zoezi la kuwasajili makurutu wanaojiunga na jeshi.

Kahariri alisema afisa yeyote wa jeshi atakayehusika au kushiriki katika zoezi la kuwahadaa wananchi kwa kisingizo cha kuwasajili kwa Vikosi vya Ulinzi, ataachishwa kazi mara moja.

Jenerali huyo aliwakumbusha maafisa wa KDF kwamba zoezi la kuwasajili makuruku halitozwi malipo yoyote, na linatekelezwa kuambatana na sheria, huku akisisitiza kuwa uadilifu na nidhamu zinasalia kuwa nguzo muhimu za huduma za kijeshi.

“Uwazi wakati wa zoezi la mwaka huu la usajili wa makurutu,, litaimarisha imani ya umma kwa Vikosi vya Ulinzi. Mchakato wenye usawa na wa kuaminika utahakikisha waliohitimu wanajiunga nasi,” alisema Jenerali Kahariri.

Alitoa wito kwa umma kutoa ripoti zozote za kutiliwa shaka wakati za shughuli ya usaili wa makurutu.

Wakati huo huo, Jenerali Kahariri aliwahimiza wanajeshi na wananchi kwa jumla kukumbatia upanzi wa miti, kama jukumu lao la kuhifadhi mazingira.

Aliyasema hayo Jumanne, kabla ya maadhimisho ya siku ya Vikosi vya Ulinzi ya mwaka huu katika kambi ya kijeshi ya Moi, Eldoret kaunti ya Uasin Gishu.

Maadhimisho hayo huandaliwa kuwakumbuka wanajeshi walioangamia wakiwa kazini pamoja na mchango wa KDF kufanikisha amani, usalama na maendeleo katika jamii.

Share This Article