Wanaharakati watishia kwenda kortini kufuatia maafa ya kutatanisha Malindi

Martin Mwanje
1 Min Read
Mwanaharakati Kelef Khalifa wa shirika la MUHURI

Wanaharakati wa kupigania haki za kibinadamu wametishia kuishtaki serikali kuu katika mahakama ya kitaifa kwa kile walichokitaja kama kuzembea kwake kuokoa maisha ya watu katika kijiji cha Bi Nzaro, kaunti ndogo ya Malindi, kaunti ya Kilifi.

Hii ni baada ya wao kuzuiliwa na maafisa wa usalama walipojaribu kuingia katika boma moja ambako miili sita ilipatikana imezikwa kwa kaburi la pamoja na watu wanne waliodhoofoeka kiafya kuokolewa na wengine kumi na moja kukamatwa.

Kijiji cha Bi Nzaro kiko karibu na eneo la Shakahola ambako mhubiri tata Paul Mackenzie alidaiwa kuwarai wafuasi wake kufunga mulo hadi kufariki, jambo ambalo lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 420 mwaka wa 2023.

Wanaharakati hao wakiongozwa na Francis Auma, Kelef Khalifa wa MUHURI, Mathias Shipeta na Hussein Khalid wa Haki Afrika na Walid Sketi wa Voice Africa walisema kuwa wataiomba mahakama itoe agizo la kufukua maiti katika shamba hilo la Bi Nzaro.

Share This Article