Wanaharakati wa Kenya Nicholas Oyoo na Bob Njagi wanaodaiwa kutekwa nyara wakiwa nchini Uganda kwa zaidi ya mwezi mmoja waliachiliwa huru.
Wawili hao ambao walikuwa wamesafiri hadi nchi hiyo jirani kuunga mkono Bobi Wine kwenye kampeni zinazoendelea, waliachiliwa kufuatia majadiliano ya kidiplomasia kati ya Kenya na Uganda.
Walichukuliwa yapata wiki sita zilizopita kutoka kwenye kituo kimoja cha mafuta katika eneo la Kireka karibu na jiji la Kampala, ambapo wanaume wanne waliwaingiza kwenye gari kwa fujo na kuondoka nao.
Katibu wa masuala ya nchi za kigeni Korir Sing’oei alithibitisha jana kwamba wawili hao waliachiliwa Ijumaa usiku na sasa wako nchini Kenya.
Balozi wa Kenya nchini Uganda Joash Maangi anaripotiwa kupokezwa wawili hao na kuwasafirisha hadi mjini Busia kwenye mpaka kati ya Kenya na Uganda ambapo walipokelewa na kamishna wa kaunti ya Busia, Chaunga Mwachaunga.
Bobi Wine alichapisha habari njema za kuachiliwa kwa marafiki wake akisema, “Baada ya siku 39 za kuzuiliwa bila mawasiliano na huku wakiteswa, ndugu zetu wakenya Bob Njagi na Nicholas Oyoo wameachiliwa huko Busia.:
Kulingana na Wine, wawili hao walimwambia kwamba walikuwa wamezuiliwa na mwana wa Rais Museveni katika kituo cha wanajeshi cha Kasenyi, ambapo walihojiwa kuhusu walichokwenda kufanya nchini Uganda.