Kundi la maafisa wa usalama kutoka asasi mbali mbali eneo la Malindi, wamemtia nguvuni Abdalla Matano Abdalla almaarufu Dalla, anayedaiwa kuwa kiongozi wa genge hatari la wahalifu.
Baada ya kukamatwa, Dalla aliwapeleka maafisa hao hadi maeneo ya NAT na Kwa Famau eneo la Maweni, ambapo washirika wake saba walikamatwa.
Waliokamatwa ni pamoja na Cosmos Kesi Kalama (almaarufu Bweko), Erick Alex Lewa (almaarufu Generali), Edwin Ondiro Onyonyi (almaarufu Last), Simon Alex Kalama (almaarufu Desai), Joseph Masha (almaarufu Thee), Moses Kwicha Mzee (almaarufu Timoteo), na Salim Ali Safari (almaarufu Mzukulu).
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, washukiwa hao ni wanachama wa genge hatari linalojulikana kama “Team Nati Dread”, ambalo limekuwa likiwahangaisha wakazi wa eneo hilo.
Washukiwa hao kwa sasa wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi, wakisubiri kufikishwa mahakani.