Walimu wapinga uteuzi wa Migosi kama waziri wa elimu

Marion Bosire
2 Min Read

Walimu kupitia chama chao cha KNUT wamepinga uteuzi wa Julius Migosi Ogamba kama waziri wa elimu nchini wakisema kwamba sekta hiyo inahitaji mtaalamu wa masuala ya elimu.

Julius Migosi Ogamba ni wakili na viongozi wa chama cha KNUT wanahisi kwamba huenda akakosa ujuzi unaohitajika katika kuendesha sekta ya elimu nchini ambayo kwa sasa inakumbwa na changamoto nyingi.

Wakiongozwa na naibu wa pili wa mwenyekiti wa kitaifa wa KNUT Agrey Namisi, walimu hao wanaelezea kwamba hawana tatizo na mtu aitwaye Migosi ila wanatilia shaka ufahamu wake wa sekta ya elimu.

Akizungumza huko Eldoret jana, Namisi ambaye alihudhuria mkutano wa mwaka wa wanachama wa KNUT tawi la Chepkoilel, alisema kwamba sekta ya elimu inahitaji mtu aliye na ujuzi na ambaye ataanza mara moja kushughulikia mabadiliko.

Namisi alikuwa ameandamana na viongozi wa tawi hilo la chama cha KNUT wakiwemo katibu mtendaji Sammy Bor.

Walimu hao wanasema utekelezaji wa mtaala wa umilisi CBC umefikia kiwango muhimu sana na unahitaji waziri aliye na ujuzi wa jinsi ya kusonga mbele.

Kulingana nao, serikali ya Kenya Kwanza imefika katikati ya muhula na uteuzi wa waziri ambaye hana utaalamu wa elimu utasababisha kucheleweshwa kwa mipango kadhaa.

Rais William Ruto alitangaza mawaziri wa kwanza 11 ambao amewateua kuchukua mahala pa wale ambao walisimamishwa kazi.

Migosi ameteuliwa kuwa waziri wa Elimu kuchukua mahali pa Ezekiel Machogu ambaye alikuwa mgombea mwenza wake wa ugavana kaunti ya Kisii kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Share This Article