Walaghai wa SHA taabani, orodha yawasilishwa kwa DCI

Martin Mwanje
1 Min Read

Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) pamoja na Baraza la Matabibu na Madaktari wa Meno (KMPDC) zimewsilisha orodha ya watu na taasisi zinazoshukiwa kuhusika katika njama ya kuilaghai mamlaka hiyo mabilioni ya pesa na hivyo kutatiza juhudi za serikali za kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, UHC. 

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imethibitisha kupokea faili 1,188 za washukiwa kutoka kwa SHA na KMPDC.

“Baada ya kupokea faili hizo, timu inayohusisha pande mbalimbali imebuniwa chini ya uongozi wa DCI kwa lengo la kupitia upya faili hizo haraka. Lengo la mapitio haya ni kuhakikisha wale wote waliohusika katika ulaghai wowote wa utoaji huduma za afya watafikishwa mahakamani bila kujali hadhi yao katika jamii au miegemeo yao ya kisiasa,” ilisema DCI kupitia taarifa iliyotiwa saini na Mkurugenzi wake wa Mawasiliano, John Marete Septemba 1, 2025.

“Kwa kushirikiana na asasi zingine zote za utekelezaji wa sheria, DCI imedhamiria kurejesha mali yote na rasilimali zingine zilizopatikana kwa njia ya udangaynifu.”

Hatua hiyo inakuja wakati baadhi ya viongozi wakizidi kutoa wito wa Waziri wa Afya Aden Duale kupigwa kalamu kutokana madai ya kukithiri kwa ufisadi kwenye SHA.

Duale amepuuzilia mbali wito huo akisema anapigwa vita na matapeli.

 

TAGGED:
Share This Article