Wakulima wa majani chai kutoka magharibi mwa Bonde la Ufa, wamelalamikia uwakilishi duni katika bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Chai Kenya -KTDA).
Wakulima hao wanadai kwamba mgongano wa maslahi unachangia pakubwa tofauti za mikafaa kati ya maeneo mawili ya kilimo cha chai.
Wanachama wa Kamati ya bunge la kitaifa kuhusu Kilimo na Mifugo, wakiongozwa na mwenyekiti John Mutunga, walisikiliza malalamiko hayo wakati wa ziara yao katika viwanda vya majani chai katika eneo hilo kwa madhumuni ya kuchunguza bei ya majani chai nchini Kenya.
Kulingana na wakulima wa viwanda vya kericho na Nyamira, bodi ya KTDA huwa na wanachama 12 na unakuta saba kati yao wanatoka mashariki na hilo linaathiri maamuzi yanayofanywa kwa maslahi ya wakulima wa upande wa Mashariki.
Wakulima hao sasa wanataka uwakilishi wa haki katika Bodi ya KTDA wakipendekeza kwamba wadhifa wa mwenyekiti uwe wa kubadilishana kati ya maeneo hayo mawili.
“Ilivyo sasa, tunafuata kanuni ya kuchuma majani mawili na chipukizi, lakini kwenye mnada hatuna mtu wa kututetea kwani hata madalali wanaegemea upande wa Mashariki” alisema James Koech, mkulima kutoka Tegat.
Wakulima pia walitaka kufutwa kwa mfumo wa kuainisha viwanda wakisema katika Mnada wa Chai wa Mombasa, viwanda vinawekwa katika madaraja A, B na C, jambo linaloamua mapema kiwango cha bei kitakachopatikana kwenye mnada.
“Mitazamo ya soko inafaa kushughulikiwa na kwenye mnada wa chai, chai inapaswa kupimwa bila upendeleo wowote. Tatizo kubwa ni mtazamo kwamba hakuna kitu kizuri kinachotoka Magharibi, hivyo wote wamewekwa daraja C,” alisema mkulima kutoka kiwanda cha Sanganyi.
Kamati hiyo ya bunge imehitimisha ziara ya siku mbili katika viwanda vya pande zote mbili ikiwa na malengo sawa ya kubainisha: mchakato wa kulipa wakulima malipo ya kila mwezi na mengineyo, ikiwemo mikafaa, na gharama mbalimbali zinazopaswa kufidiwa kabla ya mikafaa kulipwa.
Wabunge walikuwa makini kuelewa jinsi mikafaa inapangwa na kutolewa.
“Kupitia uchunguzi huu tunataka kubaini jinsi ada ya usimamizi, kama ilivyotengwa na sheria, inatumika kugharamia matumizi yaliyokusudiwa, ikiwa viwanda vinaruhusiwa kuzidisha kiwango kilichowekwa cha ada za usimamizi na kwa kiwango gani, pamoja na kiwango cha mzigo wa gharama unaoangukia mkulima,” alisema Mutunga kwa uongozi wa viwanda hivyo.
Kamati sasa iko tayari kualika taasisi kadhaa ikiwemo Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Bodi ya Chai Kenya, KALRO, KTDA MS, EATTA miongoni mwa nyingine, kufika mbele yake ili kuchunguza kwa undani nini hasa kinaathiri upangaji wa bei ya chai nchini Kenya.