Katika juhudi za kupiga jeki shughuli za kilimo ili kuboresha ukuaji wa uchumi, serikali ya kaunti ya Nakuru, imesambaza mbegu za alizeti kwa wakulima katika kaunti hiyo.
Usambazji huo unatekelezwa chini ya mpango uliozinduliwa wa kuwapa changamoto wakulima kukuza alizeti, wakati wa msimu ujao wa mvua za vuli.
Waziri wa kilimo wa kaunti hiyo Leonard Bor, alisema usambazaji huo unatekelezwa kupitia afisi za kilimo katika wadi, ambako wakulima wanashauriwa kukumbatia kilimo cha alizeti.
Waziri huyo alidokeza kuwa mmea huo ni maarufu kwani kuchukua muda mfupi kukomaa, ambao ni miezi mitatu na kusababisha kuwavutia wakulima.
Aliyasema hayo alipowatembelea wakulima kaunti ndogo ya Rongai, kaunti ya Nakuru.
‘’Wataalam wa kilimo wanawashauri wakulima kuhusu kuchagua mbegu bora, utayarishaji wa shamba, mbinu za upanzi usimamizi wa magonjwa na wadudu waharibifu na mbinu za uvunaji,” alisema Bor.
Waziri huyo alisema usambazaji huo wa mbegu za alizeti umefanikishwa na ushirikiano shilika la kilimo na chakula AFA.