Wakristo waadhimisha Jumapili ya matawi

Jumapili ya matawi ndiyo Jumapili ya mwisho kabla ya Pasaka

Marion Bosire
1 Min Read

Wakristo kote nchini jana waliadhimisha Jumapili ya matawi ambayo inaashiria mwanzo wa wiki takatifu kulingana na kalenda ya wakristo.

Maadhimisho hayo ya kila mwaka ulimwenguni kote huwa yanahusisha misafara ya waumini ambao hubeba matawi ya mitende kuashiria jinsi Yesu Kristo aliingia Yerusalemi kwa ushindi mkubwa.

Katika kanisa Anglikana la All Saints Cathedral jijini Nairobi, Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit alihimiza kuvumiliana kisiasa kote nchini.

Alilaumu serikali pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malala kwa utata uliotokana na mchezo wa kuigiza wa Echoes of War ulioonyeshwa na shule ya upili ya wasichana ya Butere.

Askofu Sapit alisema ni makosa kwa Malala kutumia watoto wa shule wasio na hatia kuendeleza ajenda yake ya kisiasa huku akikashifu polisi kwa kuwarushia wanafunzi hao vitoza machozi.

Sapit ameutaka uongozu wa kisiasa nchini ushughulikie hasira ambayo inadhihirishwa na wakenya ili amani na utulivu virejeshwe kote nchini.

Katika kanisa katoliki la Holy Family Basilica, Padri Simon Mwangi aliwataka waumini wasalie thabiti katika imani hata watakapojikuta wakidhulumiwa.

Jumapili ya matawi ndiyo Jumapili ya mwisho kabla ya Pasaka.

Share This Article