Wakongwe zaidi ya 100 kutoka eneo la Mwireri katika Wadi ya Umande, Kaunti ya Laikipia wamepokea msaada wa chakula na malazi unaohitajika sana, kutoka kwa shirika la International Relief for Africa.
Mpango huu wa kibinadamu, uliolenga hasa wazee walio na umri wa miaka 70 na zaidi, ulitekelezwa kwa ushirikiano na afisi ya Mama wa Taifa, Mama Rachel Ruto, kupitia mpango wa Mama Doing Good.
Kwa mujibu wa waandaaji wa zoezi hilo, wakiongozwa na Bi. Milka Muriuki ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa International Relief for Africa, mpango huu unalenga kuwafikia zaidi ya wazee 5,000 katika eneo hilo ambao wanakumbwa na changamoto za ukosefu wa chakula, matatizo ya kiafya na uhaba wa mahitaji ya msingi kutokana na uzee wao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la kugawa msaada, Bw. Koome Kiragu, mshauri wa shirika la International Relief for Africa, alisisitiza umuhimu wa kuunga mkono jamii za wazee ambao wengi wao wanaishi katika mazingira magumu bila huduma za msingi.
“Wazee mara nyingi husahaulika, ilhali wao ni miongoni mwa wale wanaohitaji msaada zaidi. Umri wao huja na changamoto nyingi kama vile kushindwa kutembea, magonjwa ya kudumu, na ukosefu wa kipato. Lengo letu ni kupunguza mzigo wao kwa kuwapatia chakula, malazi, na msaada wa kihisia,” alisema mmoja wa wawakilishi wa shirika hilo.
Wazee waliopokea msaada huo walieleza furaha na shukrani zao, wakisema kuwa msaada huo umefika wakati ambao wengi wao walikuwa wakikabiliwa na ugumu wa kupata mahitaji ya kila siku.
Waandaaji wa zoezi hilo walitoa wito kwa wadau wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuungana nao ili kupanua wigo wa mpango huu wa msaada na kuhakikisha hakuna mzee anayesahaulika