Wakenya wengi sasa wanapata huduma kwa urahisi kupitia e-Citizen, asema Ruto

Martin Mwanje
1 Min Read

Mfumo wa e-Citizen umekuwa wenye manufaa kwa mamilioni ya Wakenya wanaoweza kupata huduma mbalimbali za serikali wakiwa mahali popote ndani na nje ya nchi.

Rais William Ruto amesema Wakenya wapatao nusu milioni huingia kwenye mfumo huo kila siku wakitafuta huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na leseni za kuendesha magari, vyeti vya kuzaliwa, pasipoti na kadhalika.

Na si hayo tu. Ruto anasema mfumo huo umekuwa wenye manufaa katika ukusanyaji wa mapato huku serikali kuu ikikusanya zaidi ya shilingi bilioni moja kwa siku kupitia mfumo huo.

Ametoa mfano wa Mombasa na Kiambu akizitaja kuwa miongoni mwa kaunti ambazo zimefanikiwa kukusanya mapato mengi kupitia e-Citizen.

“Mfumo wa e-Citizen ni silaha madhubuti katika kukabiliana na ufisadi,” alisema kiongozi wa nchi wakati akizindua Kongamano la Ugatuzi 2025 linalofanyika katika kaunti ya Homa Bay.

Matamshi yake yanakuja wakati ripoti zimeashiria kuwa yamkini mamilioni ya pesa zilizokusanywa kupitia mfumo huo zimebadhiriwa.

 

Share This Article