Wakenya watakiwa kuzingatia sheria za barabarani

Mbunge wa zamani wa Lugari Cyrus Jirongo ndiye mwathiriwa wa hivi karibuni zaidi kupoteza maisha kupitia ajali barabarani.

Martin Mwanje
1 Min Read
Wakenya wametakiwa kuwa waangalifu hasa msimu huu ambapo shamrashamra za kusherehekea Sikukuu ya Krismasi zimeanza kushika kasi. 
Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni hasa ametoa wito kwa Wakenya kuzingatia sheria za barabarani na kujiepusha na uendeshaji magari wakati wakiwa walevi.
Amelalamikia ongezeko la ajali za barabarani ambazo zimeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini wakati wa msimu huu huku Wakenya wengi wakiuguza majeraha hospitalini kutokana na ajali hizo.
Katibu Muthoni aliyasema hayo katika eneo la Kisii wakati wa hafla ya kutoa shukrani ya Sabato.
Aidha, Muthoni amehusisha ongezeko la mizozo ya nyumbani na ubugiaji pombe, jambo ambalo alisema linapaswa kukomeshwa mara moja.
Kwa wale wenye uraibu wa kunywa pombe, amewasihi kuwajibika katika vitendo vyao.
Matamshi yake yanakuja wakati ambapo mbunge wa zamani wa Lugari Cyrus Jirongo amekuwa mwathiriwa wa hivi karibuni zaidi kupoteza maisha kupitia ajali barabarani.
Jirongo alifariki dunia Desemba 13 usiku baada ya gari lake kugongana ana kwa ana na basi moja lililokuwa likielekea mjini Busia, magharibi mwa nchi.
Ajali hiyo ilitokea kwenye barabara kuu ya Nairobi-Nakuru, hususan katika eneo la Karai mjini Naivasha.
Mamlaka zinazidi kutoa wito kwa Wakenya kuzingatia sheria za barabarani ili kuepusha maafa yanayoweza kuepukika wakati wa msimu huu wa sherehe.
Share This Article