Wakenya watakiwa kujiandikisha kama wapiga kura

IEBC itaendesha zoezi la usajili wa wapiga kura katika maeneo bunge yote 290 isipokuwa maeneo ambako kutaandaliwa chaguzi ndogo Novemba 27.

Martin Mwanje
3 Min Read
Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku akiwa na Makamishna wa IEBC wakati wa uzinduzi wa zoezi usajili wa wapiga kura

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini  (IEBC) imetoa wito kwa Wakenya kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha kama wapiga kura. 

Mwenyekiti wa tume hiyo Erastus Ethekon ameyasema hayo wakati akizindua zoezi la usajili endelevu wa wapiga kura lililoanza leo Jumatatu kote nchini.

IEBC inasema itaendesha zoezi endelevu la usajili wa wapiga kura katika maeneo bunge yote 290 na vituo 57 vya Huduma Centre ili kuhakikisha watu wengi wanajisajili.

Wale wanaotaka kuhamisha au kurekebisha kura zao watashughulikiwa katika ofisi za maeneo bunge nchini, isipokuwa maeneo ambako kutaandaliwa chaguzi ndogo baadaye mwaka huu.

IEBC inalenga kuwasajili hadi wapiga kura milioni 28.5 kufikia mwaka 2027.

Uzinduzi wa usajili wa wapiga kura ulifanyika katika kaunti ya Kajiado na kuhudhuriwa na Gavana Joseph Ole Lenku miongoni mwa mwaafisa wengine.

Ethekon akiwasihi vijana hasa kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha kama wapiga kura kwani mustakabali wa nchi u mikononi mwao.

Ni kauli zilizoungwa mkono na Gavana Lenku.

“Hakuna mpiga kura anayestahiki anapaswa kuachwa nyuma. Tunapaswa kufanya uandikishaji kama mpiga kura kufikiwa na wote na kwa urahisi ili mtu yeyote asiachwe nyuma,” alisema Lenku wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo.

“Natoa wito kwa kwa kila kijana aliyetimiza umri wa miaka 18 kutumia fursa hii na kujiandikisha. Kura ni nguvu yako, na nguvu yako inaanza kwa kujisajili.”

Awali, IEBC katika tangazo lake ilisema kuwa zoezi hilo litafanyika katika afisi zote za maeneo bunge nchini, isipokuwa maeneo yanayotarajiwa kufanya chaguzi ndogo.

Kwa mujibu wa tume hiyo, zoezi hilo ni sehemu ya jukumu lake la kudumisha daftari la wapiga kura lililo na taarifa za hivi punde za wapiga kura na la kuaminika, ambalo ni nguzo muhimu ya mchakato wa uchaguzi ulio wazi na jumuishi.

Huduma zitakazotolewa wakati wa zoezi hilo ni pamoja na usajili mpya wa wapiga kura, urekebishaji au uingizwaji wa taarifa za mpiga kura za hivi punde, uhamisho wa usajili hadi eneo lingine la uchaguzi na uhakiki wa taarifa za mpiga kura.

Huku hayo yakijiri, IEBC inaendeleza mchakato wa kuandaa chaguzi ndogo katika maeneo mbali mbali nchini ambazo zimepangiwa kuandaliwa kwa pamoja Novemba 27, 2025.

Share This Article