Msemaji wa serikali Isaac Mwaura ameonya dhidi ya uchochezi akisema kwamba serikali haitakubali nchi hii itumbukie katika vurugu kutokana na matumizi mabaya ya habari na watu wachache.
Akizungumza jana hapa Nairobi katika uzinduzi wa kitabu kiitwacho “Dirty Game” chake Peter Kipkurui, Mwaura alikanusha madai ya Diana Gichengo, ambaye ni mratibu wa kitaifa wa wa taasisi ya uwajibikaji wa kijamii TISA kwamba afisi yake hupatiwa shilingi bilioni 36.
Mwaura alisema kwamba ufadhili wa afisi yake kutoka kwa serikali hata haufiki milioni 100 akiongeza kusema kwamba serikali itachunguza wanaoisema vibaya serikali kwenye mitandao ya kijamii.
Msemaji huyo wa serikali wakati huo huo ametoa wito kwa wakenya kuendelea kutoa maoni yao kuhusu mswada wa fedha wa mwaka 2025 kupitia njia faafu akisema serikali haitakubali tukio jingine la mswada wa fedha kama la mwaka jana.
Mwaura alikuwa mgeni wa heshima katika uzinduzi wa kitabu hicho cha Peter Kipkurui wa umri wa miaka 26 pekee aliyefuzu kutoka chuo kikuu cha Kenyatta.
Katika uzinduzi huo Mwaura alishangaa ni nini cha mno kuhusu siasa na iwapo mtu anaweza kudumisha maadili na kusalia mkweli katika wito wa uongozi.
Mwaura alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa akiwemo mbunge wa Emgwen Josses Lelmengit katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa maktaba ya kitaifa.