Wakenya wahimizwa kukumbatia amani na umoja uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia

Marion Bosire
2 Min Read

Wakenya wamehimizwa wakumbatie amani, upendo na umoja, nchi hii inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Akizungumza katika Kauti Ndogo mpya ya Abogeta, Kaunti ya Meru, katika ibada kwenye makao makuu ya Kauti hiyo Ndogo, Naibu Kamishna Richard Tuwei, alihimiza wakazi na Wakenya kwa jumla kuonyesha upendo msimu huu wa sikukuu na zaidi wanapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.

Tuwei alisema maombi hayo yaliyowaleta pamoja wakazi, viongozi wa maeneo, viongozi wa dini na wafanyakazi wa Kauti Ndogo, yalilenga kutafuta uingiliaji wa Mungu wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Aliwataka wakazi na Wakenya wote kuonyeshana upendo.

Kauli za Tuwei ziliungwa mkono na Padre wa Kanisa Katoliki, Raphael Raing’oi, ambaye aliwataka wakazi na Wakenya kuonyesha upendo, amani na umoja si tu wakati wa msimu huu wa sikukuu bali pia nchi inapokaribia uchaguzi mkuu wa 2027.

Padre huyo alisema ibada hiyo itaendelea kufanyika kila mwisho wa mwaka katika makao makuu ya Kauti Ndogo ya Abogeta, ikiwa na lengo la kuwaleta watu pamoja kutafuta uingiliaji zaidi wa Mungu.

Alisema kuwa, kutokana na kuundwa kwa Kauti Ndogo mpya ya Abogeta, kama wakazi walifurahia hatua hiyo kwa sababu inaleta huduma karibu zaidi na wananchi.

Fr. Raphael aliwahimiza wakazi kuendelea kuyaombea serikali za kaunti na taifa, wanasiasa na nchi kwa ujumla.

Tukio la leo linaweka historia mpya kwani uongozi wa Kauti Ndogo mpya ya Abogeta, wakazi na viongozi wa dini walikusanyika pamoja kwa ajili ya maombi.

Share This Article