Wakenya wahimizwa kujiepusha na ufisadi

Tom Mathinji
1 Min Read

Jaji mkuu Martha Koome amewaomba wakenya wasipotoshwe kutoa hongo iwapo watakamatwa kutokana na makosa ya kukiuka sheria za usalama  barabarani.

Akizungumza katika majengo ya Mahakama ya Upeo hii leo Jumatatu, Koome alisema serikali kwa ushirikiano na mashirika kadhaa ya haki na yale ya kiusalama, iliafikiana kutumia mbinu ya pamoja iliyoratibiwa ili kuimarisha usalama wa barabarani kote nchini.

Koome alisema hatua hizo zinakusudiwa kuzuia vifo vinavyotokana na ajali za barabarani akisema katika visa vingi, waathiriwa ni watembeaji wasiokuwa na hatia au waendeshaji magari ambao huathiriwa na makosa ya watumiaji wengine wa barabara.

Jaji mkuu alionya kwamba ukiukaji wa sheria za barabarani, hasa kuendesha magari kwa kasi huongezeka wakati wa safari za msimu wa sherehe.

Koome alitangaza kwamba mahakama tamba zitaanzishwa  ili kushughulikia haraka kesi za trafiki wakati huu wa msimu wa sherehe.

Kundi la pamoja na ushirikiano wa umma utahitajika kote nchini ili kuhakikisha usafiri salama  wakati huu wa msimu wa sherehe na baadaye.

TAGGED:
Share This Article