Wakenya milioni 1.5 kulipiwa SHA na serikali

Rais William Ruto amesema Wakenya watakaolipiwa michango yao na serikali kuu kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA ni wale wasiojiweza kifedha.

Martin Mwanje
2 Min Read

Serikali itawalipia Wakenya milioni 1.5 michango yao kwa Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA kuanzia wiki ijayo.

Rais William Ruto amesema Wakenya hao ni wale wasiokuwa na uwezo wa kulipa michango yao kwa mamlaka hiyo.

Ruto pia amesema hivi karibuni atakutana na Magavana na wabunge ili wao pia wawalipie Wakenya wengine milioni moja michango yao.

Ameelezea kuwa michango kwa SHA ni yenye usawa wa asilimia 2.75 ya mapato, hatua ambayo amesema imeiwezesha serikali kupata fedha za kutosha kuwachangia wale wasiokuwa na uwezo wa kulipa.

“Kinyume cha NHIF, iliyogharimia wale wanaojiweza na wale waliokuwa na ajira, SHA ni ya Wakenya wote. Huduma za matibabu si za watu wachache; ni za Wakenya wote,” alisema kiongozi wa nchi.

Aliyasema hayo alipokutana na viongozi wa mashinani kutoka kaunti ya Turkana katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.

Rais alitoa wito kwa viongozi hao kuongeza kasi ya kujiandikisha kwa SHA ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma nafuu za matibabu na za ubora wa juu kwa kila kaya.

Ameongeza kuwa malipo ya SHA yanatumwa kwa hospitali mahususi wala siyo kaunti kama ilivyokuwa awali.

Hatua hiyo inadhamiriwa kuhakikisha vituo vya matibabu vinaweza vikatoa huduma bora za matibabu.

Kwa mara nyingine, Ruto alizionya zahanati, vituo vya afya na hospitali za kaunti ndogo dhidi ya kuwatoza ada wagonjwa wa kutibiwa na kurejea nyumbani akisema serikali imetenga shilingi bilioni 21 za kugharimia matibabu yao.

Alisema malipo hayo yatatolewa kupitia SHA.

 

 

Share This Article