Wakenya kupewa vitambulisho vya taifa bila malipo

Tom Mathinji
1 Min Read
Wakenya kupokea vitambulisho vya taifa bila malipo.

Vijana wanaohitimu umri wa miaka 18 hapa nchini, sasa wana sababu ya kutabasamu kwa kuwa watapokea vitambulisho vya taifa bila malipo yoyote.

Akiwahutubia wananchi leo Alhamisi katika mtaa wa Kibra, Jijini Nairobi, Rais William Ruto aliagiza kufutiliwa mbali mara moja kwa malipo ya utoaji vitambulisho vya taifa.

“Natangaza nikiwa hapa Kibra ya kwamba, kitambulisho ipatianwe bila malipo yoyote. Kila mtu apatiwe kitambulisho bila malipo na kwa mpango ambao hauna ubanguzi kwa Wakenya,” alisema Ruto.

Agizo hilo la Alhamisi linafutilia mbali agizo la hapo awali, ambapo wanaotafuta stakabadhi hiyo muhimu walihitajika kulipa shilingi 300 na waliopoteza wakitakiwa kulipa shilingi 1,000.

Mwezi uliopita, kiongozi wa taifa akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Kaskazini Mashariki mwa nchi, aliagiza kusitishwa usaili kwa wakazi wa mpakani wanaotafuta vitambulisho vya taifa.

Share This Article