Wakenya Milioni 24.8 wamesajiliwa kwa SHA, asema Duale

Tom Mathinji
2 Min Read
Makao Makuu ya SHA

Juhudi za Kenya za kufanikisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa wote, zimepiga hatua huku Wakenya Milioni 24.8 wakisajiliwa kwa Halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA).

Waziri wa afya Aden Duale amesifia maendeleo hayo, akitaja kuwa yametokana na mageuzi yaliyotekelezwa katika halmashauri hiyo.

Akizungumza leo Jumatano wakati wa kikao na wanahabari katika Makao Makuu ya SHA Jijini Nairobi, Duale alifichua kwamba ufanisi huo umechangiwa na kampeni kabambe za usajili katika kaunti.

Kulingana na waziri Duale, wakenya milioni 4.5 wamepokea matibabu ya magonjwa ya kawaida na huduma za uzazi, kupitia hazina ya huduma za msingi, huku wakenya milioni 2.2 wakinufaika kutokana na huduma maalum, wakiwemo wagonjwa elfu 8 wanaopokea matibabu ya figo na elfu 18 wanaotibiwa saratani.

Aliongeza kwamba visa elfu 550 vya kujifungua vimeshughulikiwa tangu Oktoba mwaka jana. Kufikia sasa, Duale alisema, shilingi bilioni 6.8 zimelipwa chini ya malipo ya matibabu ya huduma za msingi, huku shilingi bilioni 1.5  zikitazamiwa kulipwa wiki ijayo.

Aidha alitoa wito kwa wakenya kutoa ripoti kuhusu malipo yasiyo halali katika vituo vya matibabu vya serikali, akisisitiza kwamba shilingi  bilioni 13 zimetengwa kufadhili matibabu ya huduma za kimsingi bila malipo katika hospitali za ngazi ya Level 2 hadi Level 4.

Duale alisema amepokea ripoti kutoka tume huru iliyochunguza sakata ya uuzaji na upandikizaji figo.

Share This Article