Huduma ya taifa ya Polisi NPS imehakikishia umma kuhusu usalama katika eneo la biashara la katikati la Nairobi, kufuatia ripoti ya vyombo vya habari iliyoangazia madai ya hali ya kutokuwa salama katika eneo hilo.
Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari NPS ilithibitisha tukio lililotokea siku ya Ijumaa, Agosti 22, 2025, katika jengo la Nanak House.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa polisi, shambulio dhidi ya biashara nne ndani ya jengo hilo halikuwa tukio la kiholela, bali lilihusishwa na mzozo wa ndani wa kiraia, ambao tayari uko mahakamani.
Polisi wamethibitisha kukamatwa kwa mtu mmoja, huku hatua zaidi zikitarajiwa kuchukuliwa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Nairobi alitoa taarifa hizi, akisisitiza kuwa eneo la katikati mwa jiji la Nairobi ni eneo salama zaidi kwa shughuli za kibiashara.
“Eneo la katikati mwa jiji ni alama ya uhai wa jiji la Nairobi na bado ni salama kwa kila mtu” ilisema taarifa iliyotiwa saini na hatibu wa polisi Muchiri Nyaga.
Polisi pia walipongeza hali ya jumla ya usalama nchini, wakihusisha mafanikio hayo na oparesheni madhubuti pamoja na ushirikiano mzuri kutoka kwa umma.