Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amehakikishia wakazi wa Meru wanaokumbwa na wizi wa mifugo na ujambazi, usalama wao.
Waziri huyo wa usalama wa ndani alisifia kazi inayofanywa na polisi wa akiba wa kitaifa – NPR katika kupambana na visa vya wizi wa mifugo na ujambazi katika mpaka wa kaunti ya Meru na kaunti jirani.
Murkomen alisema wizara yake inafanya kazi kwa bidii kukabiliana na visa vya ukosefu wa usalama nchini.
Kamishna wa Kaunti ya Meru, Jacob Ouma alisema kaunti ya Meru imekuwa ikiathirika wa wizi wa mifugo na ulanguzi wa dawa za kulevya kutoka nchi jirani na kama maafisa wa usalama wanafanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo hilo.
Gavana wa Kaunti ya Meru, Isaac Mutuma, alisema kama serikali ya kaunti wako tayari kushirikiana na serikali kuu katika masuala ya usalama ndani ya kaunti hiyo.
Kufuatia visa vya mara kwa mara vya migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, gavana huyo wa Meru alihimiza serikali kuu kufidia waliothirika na migogoro hiyo.
Mutuma aliunga mkono hatua ya kuongeza idadi ya polisi wa akiba wa kitaifa (NPR) akibainisha kuwa kwa miaka mingi kaunti ya Meru imekuwa kama “ATM” ya wizi wa mifugo.