Wakazi wa mtaa wa Majengo waliokuwa na hasira, leo Jumatano walivamia na kuwasha moto katika kituo cha polisi cha Shauri Moyo, wakilalamikia mauaji ya mvulana wa kidato cha tatu.
Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 17, anadaiwa kupigwa risasi na afisa wa polisi Jumanne usiku, wakati maafisa hao walipokuwa wakishika doria.
Wakati wa maandamano hayo, magari mawili ya polisi yaliteketezwa, huku baadhi ya nyumba za maafisa hao zikochomwa.
Afisi ya chifu wa eneo hilo pia haikusazwa, kwani pia iliteketezwa, waandamanaji hao wakishinikiza hatua zichukuliwe dhidi ya afisa aliyemuua mvulana huyo.
Kisa hicho kilisababisha msongamano mkubwa wa magari huku biashara nyingi zikilazimika kufungwa.
Wahudumu wa afya kwenye eneo hilo wmaeripoti kutibu waathiriwa mbalimbali waliokuwa na matatizo ya kupumua na majeraha madogo.
Maafisa zaidi wa polisi wamepelekwa kwenye eneo hilo katika juhudi za kurejesha amani.
Viongozi wa kijamii wametoa wito wa utulivu huku wakihimiza pande mbili husika kutulia na kuruhusu mashauriano ili kuepusha umwagikaji zaidi wa damu.