Wakazi wa Eneo Bunge la Kiminini, Kaunti ya Trans Nzoia, leo walijitokeza kwa wingi kueleza hisia zao za kuunga mkono pendekezo la kurekebisha Katiba ili kukita katika katiba hazina muhimu ambazo ni ile maendeleo ya maeneo bunge – NG-CDF, ya uwezeshaji wa wanawake -NGAAF na hazina ya usimamizi ya Seneti.
Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Shule ya Msingi ya Kiminini uliangazia wito wa kutetea na kudumisha hazina hizo, ambazo wakazi walisema zimeleta maendeleo makubwa katika sekta za elimu, miundombinu, ustawi wa jamii na huduma za msingi.
Mbunge wa Kiminini Kakai Bissau alitaja hazina ya NG-CDF kuwa kichocheo cha heshima, upatikanaji wa huduma na fursa, akilitaka bunge kuweka kando siasa na kutenda lililo sahihi kwa ajili ya wananchi.
“Hazina hii sio hisani kwa wananchi ni haki yao. NG-CDF imewapeleka watoto darasani, imeleta maji nyumbani na fursa vijijini ambavyo vilisahaulika. Kuweka mfuko huu ndani ya Katiba ni njia ya kulinda mafanikio haya kwa vizazi vijavyo” alisema Bissau.
Mzee Enos Kisiangani mkazi aliyesomea shule ya msingi ya Kiminini mwaka wa 1968, alisema ameshuhudia mabadiliko ya moja kwa moja yaliyotokana na hazina ya NG-CDF.
“Nilisomea shule ya msingi ya Kiminini 1968 na haikuwa hivi. Mheshimiwa Bissau umebadilisha maisha ya watoto wetu” alisema mzee huyo.
Emmaculate mwanafunzi katika shule hiyo alisema hazina hiyo imewezesha upatikanaji wa maji, ujenzi wa miundombinu ya walemavu, viwanja vya michezo na chumba cha walimu. “Inatusaidia kusalia shuleni. Inapaswa kuendelea” alisema.
Michelle mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Andrews Baraton, alisema ufadhili wa masomo unaotolewa na hazina ya NG-CDF umezuia wengi kuacha shule wakati pesa za serikali zinapochelewa.
“CDF inatufanya tusalie shuleni. Siku hizi, wasichana wengi wanafika chuo kikuu na mimba za mapema zimepungua” alisema.
Mzee Wanyama alikuwa na ujumbe wa moja kwa moja kwa wanaopinga hazina hiyo, “Mtu mwenye anaota ndoto za mchana za kuondoa CDF hajui maana ya CDF. Watoto wetu wamepata elimu kutoka CDF. Wao ndio wanakuja kuinua jamii.”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Protus Juma aliyegusia changamoto za awali akisema, “Kitambo mtoto akifika darasa la nane, hawezi songa mbele. Sasa, CDF inawapeleka hadi shule ya upili. Iendelee.”
Mkuu wa shule, Lucy Shirandula, alisifu mchango wa hazina hiyo katika kupunguza mzigo kwa wazazi na kuwezesha elimu bora.
“CDF imejenga maabara za sayansi, barabara, mabweni na madarasa. Imebadilisha maisha na kupunguza mzigo wa wazazi. Naiunga mkono kikamilifu iendelee.” alisema mkuu huyo wa shule.
Kwa hisia kali, Emily ambaye ni mama wa umri mdogo alisema, “CDF imetusongeza mbele na mwenye macho haambiwi tazama”.
Kadri mjadala wa kitaifa kuhusu kuingizwa kwa hazina hizo kwenye Katiba unavyoendelea, ujumbe kutoka Kiminini uko wazi: maendeleo ni lazima yalindwe na sauti ya mashinani haipaswi kupuuzwa.
“CDF iendelee, wasijaribu kunyonga” mkazi mmoja alimalizia.