Wakazi wa maeneo ya Kiroe na Micobo, wadi ya Ndeiya, eneo bunge la Limuru kaunti ya Kiambu, wanaishi kwa hofu baada ongezeko la visa vya wezi wa mifugo.
Kulingana na wakazi hao, ng’ombe wawili wameibwa chini ya muda wa wiki moja, na kusababisha wasiwasi ikizingatiwa kuwa wao huwategemea mifugo kujikimu kimaisha.
Wanavijiji hao walisema wahalifu hao hulenga makazi ya wakongwe, ambao hawana uwezo wa kukabiliana na wezi na mabo chanzo cha mapato yao ni mifugo.
Wametoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka haswa kuweka kituo cha polisi katika eneo la Micobo ili kukabiliana na visa vya uhalifu.
Aidha walilalamikia ukosefu wa doria za polisi, wakisema hatua hiyo pia imechangia kuongezeka kwa visa vya uhalifu.